Nasema nao Wavyele

Muwapi wenye hekima, mlokuwa zama zile
Twawaita kwa hishima, njooni enyi wavyele
Wanawenu tumekwama, kifikira wachochole
Tufunzeni yalo mema, mlofunzwa ninyi kale.

Muwapi ninyi wajuzi, mlofundwa zama hizo
Mlokanywa na wazazi, na kupewa makatazo
Njooni mtupe kozi, mtoe huu uozo
Maana hiki kizazi, kimejawa matatizo.

Muwapi wataalamu, muwezao kutufunda
Mlojawa ufahamu, mtufunze mlo tenda
Njooni mutoe sumu, twajua munatupenda
Maana hii kaumu, mambo yetu yamipinda

Muwapi wanye adabu, busara kama za kadhi
Mtupe leo jawabu, mufanye yenu faradhi
Mnene kama mababu, tupate nasi waadhi
Wenzenu twapata tabu, imishuka yetu hadhi.

Muwapi nyie miamba, muwezao kutujenga
Mulitoe letu vumba, hino linalotuzonga
Hatuwezi kujigamba, kwenye kiza twajigonga
Sitanii nawaomba, na kaditama nafunga.

© Kinyafu Marcos, 2019
Dar es salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!