Umeniacha Mwandani

Nakupenda, wangu mleta-amani,
Umetenda, mengi yasiyo kifani,
Nitakonda, siha nikose mwilini,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Umeunda, nyingi raha mtimani,
Limetanda, sikitiko la huzuni,
Hujadinda, muhibu kuniauni,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Unadunda, moyo hauna hisani,
Ulikanda, mwili wangu kuubuni,
Langu tunda, kaanguliwa mtini,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Hujaenda, unitie tatizoni,
Miye kinda, kaniacha kiotani,
Umepanda, ukenda zako ngazini.
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Langu banda, umelitia jichoni,
Umependa, umetaka ukwasini,
Umetenda, kanitia maafani,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Menishinda, mahaba huyabaini,
Umedinda, muhibu kuniamini,
Ukatenda, hilo la uhayawani,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Umeranda, ukaenda faraghani,
Kunipenda, si kuniacha mwendani,
Ka’ ni rinda, takupeleka dukani,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Nakupenda, ela una walakini,
Hutokwenda, kulima huko kondeni,
Nina gunda, hutaki zangu kanuni,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Nakupenda, sitokuacha mwendani,
Nitarunda, wenendapo mafichoni,
Ndugu donda, litaniweza moyoni,
Umekwenda, umeniacha mwendani.

Nakupenda, sipendi kwenu nyumbani,
Wanitenga, usemapo baitini,
Nitatenda, ujapo mwangu chumbani,
Umekwenda, uniacha mwandani.

Nakupenda, sitoufanya uhuni,
Takulinda, tupige soga chumbani,
Yatawanda, mahaba yasiwe duni,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Nakupenda, mrembo nakubaini,
Umeshinda, wewe wangu nakwamini,
Menipanda, uzuzu mwangu kichwani,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Umedinda, kunitoroka mwandani,
Yakupanda, ya hasira akilini,
Kwake nenda, mwambie aje chumbani,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

Liko rinda, nitakupa la thamani,
Kurandanda, wacha tuende nyumbani,
Lipo banda, tatufaa kijijini,
Umekwenda, umeniacha mwandani.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!