Tetemo Zizimo

Tetemo zizimo ndimo, ndimo tetemo lilimo,
Tetemo latoa somo, zizimo ndimo tetemo,
Tetemo chukuliano, tetemo hangaikano.

Ajira chele hazimo, tetemo kimya midomo,
Jamii hasi kilimo, njaa lilo kubwa domo,
Tetemo chukuliano, tetemo hangaikano.

Tetemo ziwani limo, nchi kukosa mfumo,
Dunia kuwa kifumo, fumo maisha zizimo,
Tetemo chukuliano, tetemo hangaikano.

Zizimo moyoni mwamo, faraja zangu hazimo,
Tetemo halina komo, daima latoa somo,
Tetemo chukuliano, tetemo hangaikano.

Tetemo la kanisani, kifo hitimo hisani,
Lakuvunda ni ubani, zizimo hisia tani,
Tetemo chukuliano, tetemo hangaikano.

Tetemo chukuliano, tetemo kubwa agano,
Tetemo hangaikano, tetemo lang’oa meno,
Tetemo halina ono, elekezo pasi kono.

Zizimo ndilo tetemo, zizimo huwa ulimo,
Zizimo tumboni limo, zizimo kaburi pimo,
Zizimo pia tetemo, lenye hisia simamo.

Tetemo mahakamani, zizimo kubwa tetemo,
Tetemo za kizimbani, zizimo oneo limo,
Tetemo halina ono, elekezo pasi kono.

Tikisiko la zizimo, aridhi kuwa tetemo,
Michuwano kwa midomo, miili anguko pimo,
Zizimo pia tetemo, lenye hisia simamo.

Nafsiyo i tetemo, hatiani mimi simo,
Milele fumbo la domo, akilini finyu pimo,
Tetemo halina ono, elekezo pasi kono.

Tetemo shikiriano, kwa wenye mahusiano,
Tetemo kubwa kiuno, miili yenye mavuno,
Tetemo halina ono, elekezo pasi kono.

Tetemo la msimamo, tetemo kubaliano,
Msimamo wa tetemo, athari mifarakano,
Zizimo pia tetemo, lenye hisia simamo.

Tetemo la migodini, aridhi kufumba mboni,
Tetemo la ofsini, maisha kabali duni,
Tetemo halina ono, elekezo pasi kono.

Tetemo limo shuleni, jenizani kaburini,
Mimba miozo damuni, harufu ozo puani,
Zizimo pia tetemo, lenye hisia simamo.

Tetemo lilo nyumbani, baba na mama chumbani,
Tetemo lilo jikoni, mwiko sufuria ndani,
Tetemo halina ono, elekezo pasi kono.

Tetemo la gerezani, pasi kweli hatiani,
Fumbo kwenda maishani, maisha kuwa bindoni,
Zizimo pia tetemo, lenye hisia simamo.

Zizimo bila kisomo, ubongo ni zege domo,
Maisha huenda gomo, paso damu la gugumo,
Tetemo giza ndo limo, mwangani wote hawamo

Tetemo la uwanjani, wachezaji kuwa ndani,
Tetemo la kitandani, wawili wa mwanandani,
Zizimo pia tetemo, lenye hisia simamo.

Zizimo ni chomochomo, vichomi kuwaka domo,
Zizimo kimya cha pimo, imani kugida kimo,
Tetemo halina ono, elekezo pasi kono.

Tetemo dole viwili, kwa wakwanza na wapili,
Tetemo pia ni dili, misuli inayojali,
Zizimo pia tetemo, lenye hisia simamo.

Zizimo huwa dhahiri, mioyo ilo jasiri,
Zizimo hutoa siri, zilizochimba bahari,
Tetemo halina ono, elekezo pasi kono.

Tetemo kono dahari, kono la wanafahari,
Tetemo huwa vizuri, kusakanya pondo dori,
Zizimo pia tetemo, lenye hisia simamo.

Hitimo lanusurika, kutetema kuanguka,
Zizimo lahangaika, kuchachafya Afrika,
MUNGU we wahitajika, wanao kunusurka.

Rekodi inavunjika, karatasi kuchanika,
Kalamu inavunjika, wino hunakorezeka,
Zizimo kwa Afrika, ni tetemo lisofika.

Tetemo layaanika, zizimo pia kunuka,
Tetemo likiinuka, zizimo lanusurika,
Tetemo kwa mwafrika, ni zizimo lisofika.

Zizimo linayashika, makusudio ya nyika,
Zizimo hukasirika, kwa dodoso za kutoka,
Zizimo kwa Afrika, ni tetemo lisofika.

Nawaona wachafuka, tetemo vumbi funika,
Nasikia watafika, tetemo njia tandika,
Tetemo kwa mwafrika, ni zizimo lisofika.

Zizimo ama nukio, kimya ndani kusudio,
Tetemo ni jaribio, tambozo kwa nzao zao,
Zizimo kwa Afrika, ni tetemo lisofika.

Tetemo huwa ni zingwe, ukiamuwa utengwe,
Tetemo sema ujengwe, kwa aibu na upingwe,
Tetemo kwa mwafrika, ni zizimo lisofika.

Abed Anthony
(Shimbolyo)

Maoni 1

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!