Ninangu

Pongezi ni kwako mama, kunileta duniani,
Jukwani ninasimama, nao ukweli wa ndani,
Kama sio wewe mama, ngetoka wapi jamani?
Ninangu heri nakupa, kunileta duniani.

Maziwayo linyonyesha, nilipopatwa na njaa,
Mazuriyo lionyesha, nisije kupata balaa,
Mama, kweli unatosha, ya nini kukuhadaa?
Ninangu heri nakupa, kunileta duniani.

Dunia ina makubwa, mazuri ninayoona,
Rafiki zangu wakubwa, twacheza kikimbizana,
Kichoka twanywa ubwabwa, uliopikwa na NINA,
Ninangu heri nakupa, kunileta duniani.

Mamangu nimemaliza, machache nimeyasema,
Narudi kujituliza, kiwaza kukupa mema,
Mazuri nikiyajaza, waama sitakunyima,
Ninangu heri nakupa, kunilea duniani.

© Cornelius Barasa

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!