Kilio cha Mkulima

Nawatafuta mafundi, wajuzi wa hii fani,
Shamba langu la mahindi, limevamiwa na nyani,
Wanakuja kwa makundi, tena wazi hadharani,
Mkulima nina tabu, shamba kavamia nyani.

Sio kwamba sililindi, jamani nieleweni,
Nimewategea gundi, wakija wanase chini,
Cha ajabu hawagandi, sijui ati kwanini,
Mkulima nina tabu, shamba kavamia nyani.

Nipendalo silitendi, moyo hauna amani,
Hata mgongo sipindi, kisa nahamia nyani,
Ila kushinda sishindi, sasa nipo taabani,
Mkulima nina tabu, shamba kavamia nyani.

Tabia hii sipendi, kweli nasema jamani,
Mbele kuenda siendi, nyani kwangu mtihani,
Kupanda sasa sipandi, kazi haina thamani,
Mkulima nina tabu, shamba kavamia nyani.

Chozi li kama kilindi, nalia pasi kifani,
Bora niuze mtindi, kilimo ki mashakani,
Lile shamba la Mufindi, nitawapa majirani,
Mkulima nina tabu, shamba kavamia nyani.

© Kinyafu Marcos,2018.
Dar es salaam, Tanzania.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!