Mke Mwema

Mke mwema yupo wapi, wajuzi nawauliza,
Nitamtambua vipi, suali lanitatiza,
Ama sifaze ni zipi, nambieni maajuza,
Natafuta mke mwema, ila bado sijamwona.

Nizunguke hadi wapi, nipate anayeweza,
Nitampa hata pipi, aje kwangu niliwaza,
Ninawaza ni kwa vipi, shida nitaimaliza,
Natafuta mke mwema, ila bado sijamwona.

Wengi wao ni makapi, lulu wameipoteza,
Walishwa hawanenepi, tamaa zimewameza,
Bora tuwafunge nepi, maana wanichefuza,
Natafuta mke mwema, ila bado sijamwona.

Jama nijifiche wapi, maana kweli nawaza,
Nitumie njia zipi, tabu nipate ondoza,
Chanda chema ndio kipi, ‘meshindwa kujiongeza,
Natafuta mke mwema, ila bado sijamwona.

Nitasoma wafilipi, huenda ameeleza,
Sifa za mke ni zipi, alizosema Muweza,
Na mazuriye ni yepi, Mola aliyo mjaza,
Natafuta mke mwema, ila bado sijamwona.

Tama namaliza vipi, ila ndo nahitimiza,
Jibu sijui ni lipi, waneni mtan’eleza,
Nijue mke ni yupi, atakae nipendeza,
Natafuta mke mwema, ila bado sijamwona.

© Kinyafu marcos,2018
Dar es salaam, Tanzania

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!