Vitimbe na Sitimbe

Vitimbe hata sitimbe, anguko ndilo tandiko,
Sitimbe navyo sitimbe, tandiko navyo anguko,
Ni maisha ya malimbe, yashindayo mizunguko.

Jilambe pia utambe, ukijipiga vijembe,
Lamba utamu wa pembe, lenye chomo kali jembe,
Ni maisha ya malimbe, yashindayo mizunguko.

Anguko hilo tandiko, lenye moshi kuntu kiko,
Tandiko kilo kijiko, anguko lamba andiko,
Ni maisha ya malimbe, yashindayo mizunguko.

Kilio cha matandiko, chaniko za maandiko,
Simanzi za lalamiko, yote hayo si ya mwiko,
Ni maisha ya malimbe, yashindayo mizunguko.

Maisha usijigambe, wewe ni nyasi wa ng’ombe,
Maisha usiyalambe, kesho chungu cha kimbembe,
Ni maisha ya malimbe, yashindayo mizunguko.

Abed Anthony
(Shimbolyo)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!