Ulikuwa Sahihi

Dunia ni mwenda pole, ha’simami kwa kidole,
Kwenda kusema ya vile, aridhi kuyakodole,
Wazuo zako sahihi, nami siwezi darihi.

Maisha yote mchele, maisha ya vibwetele,
Maisha pigo gobole, maisha yoyote yale,
Wazuo zako sahihi, nami siwezi darihi.

Uliyasema kwa wale, kwangu yakaja ya vile,
Didimo zao kwa pole, hangaiko hali zile,
Wazuo zako sahihi, nami siwezi darihi.

Sahihi kweli kwa yale, uliyosema ya zile,
Tabu za walizo ole, zilizaliwa polele,
Wazuo zako sahihi, nami siwezi darihi.

Nywele nyonyoko vichele, nyusi nazo za ndulele,
Milio zao kelele, vyura wafusa tulele,
Wazuo zako sahihi, nami siwezi darihi.

Ng’ang’ano za wana wale, hangaiko zilezile,
Mungu futa chozi zile, kesho wanjaa wakale,
Wazuo zako sahihi, nami siwezi darihi.

Abed Anthony
(Shimbolyo)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!