Shimo la Siafu

Shimo mleta ya kimo, shimoni amani ndimo,
Shimo hauna kipimo, shimo unatoa somo,
Shimo la nyingi siafu, durufu za utukufu.

Shimo umetia guu, siafu kula makuu,
Kwa usemi huu huu, shimoni kuna nafuu,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Shimoni kuna kilimo, jembe zagegeda humo,
Shimoni kuna mashimo, vyuma vyaleta lalamo,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Taratibu wanukuu, domodomo za kifuu,
Siafu wakijituu, mojamoja zao puu,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Shimo la konde siafu, maliwato nyingi bifu,
Shimo mleta harufu, huna mwingi utukufu,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Kazi kazi maradufu, kunyemela utukufu,
Umoja wao wasifu, nyendo zao makinifu,
Umoja kuusaadifu,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Maarifa ni nafuu, kuyafuata ya juu,
Shimoni ni tabu tuu, hangaiko zao duu!,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Siafu wa jungu kuu, hujisifu kwa wadau,
Siafu huna makuu, ni wewe nakunusuu,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Panya nao kujitoa, mavi yao kuyazoa,
Siafu kujitogoa, nyoka nao wanandoa,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Huyabuni washindao, hitimo maisha yao,
Ukoo wa wanawao, chuki na hira ni zao,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Maisha yapo shimoni, MUNGU ndiye maishani,
Shimo hili la jangwani, binadamu matatani,
Shimo unatoa somo, kwa wendao kwa kidomo.

Abed Anthony
(Shimbolyo)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!