M’bwaga Zani

Kalamu yangu nishike, nitoe lilo moyoni,
Wengine wafaidike, tuishivyo duniani,
Yatupasa tukumbuke, kama tadunu tudani,
Kila abwagae zani, na zani hubwagwa kwake.

Bure usiyatutike, yakutupa jalalani,
Kwa mwingine ukaweke, nyumbanikwe barazini,
Mja usihadaike, kuna leo na mwakani,
Kila abwagae zani, na zani hubwagwa kwake.

Jambo lina jambo lake, ndivyo ilivyo kanuni,
Kupituka usitake,ni chanzo cha mitihani,
Twaishi kama mvuke, tahadhali tuwekeni,
Kila abwagae zani, na zani hubwagwa kwake.

Usotaka likufike, simuombee jirani,
Kila mtu ana lake, umpe lako kwanini.
Yanini uhangaike, mlipaji ni Manani,
Kila abwagae zani, na za hubwagwa kwake.

Yaloyako yafutike, uyahifadhi moyoni,
Ukae usianguke, ja mwezi ulo angani,
Kwa chupa usitupake, mafuta kwa mgongoni,
Kila abwagae zani, na zani hubwagwa kwake.

Sifa ngoja zikufike, subira ndiyo sukani,
Jua kuna siku yake, ndovu kungia mjini,
Batali muamba peke, kwenye hadhara haneni,
Kila abwagae zani, na zani hubwagwa kwake.

Kaditamati nandike, kuna mwanzo na mwishoni,
Mwisho ni budi tufike, hatukwepi ikhiwani,
Mola wetu ana yake,ufanye wewe unani?
Kila abwagae zani, na zani hubwagwa kwake.

Hamisi A.S. Kisssamvu
Baitu Shi’ri, Mabibo, Dar es Salaam

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!