Wakenya Tunaumia

Ukumbini narejea, kichwa kikiwa chauma,
Fulusi zimepotea, hatuzikimu gharama,
Gharama yatulemea, mafuta yatupa homa,
Wakenya tunaumia, mafuta yashuke bei.

Mafuta yashuke bei, tupate kuishi vema,
Wakenya tunaumia, hii kweli ni hujuma,
Mwatuhujumu haswaa, mtaki tupate mema,
Wakenya tunaumia, raisi twakulilia.

Raisi twakulilia, twataka bei kuzama,
Naomba utuokoe, pata ushuru kupima,
Kwani ndisi twaumia, kwa ya juu hi gharama,
Wakenya tunaumia, tumuombe Mola dua.

Tumuombe Mola dua, tupate maisha mema,
Serikali tulipie, madeni twache kuhema,
Nasi tujitegemee, kukopa kuna gharama,
Wakenya tunaumia, nani atatutetea?

Nani atatutetea, tutoke kwenye dhuluma,
Madeni twayalipia, tangu zamani zama,
Mbona tuwategemee, hao watu wa gharama,
Wakenya tunaumia, Serikali Saidia.

Serikali saidia, kwa kupunguza gharama,
Matumizi yapungue, kwenye serikali nzima,
Madeni tuyalipie, tupate simama wima,
Wakenya tunaumia, twalia sisi twalia.

Twalia sisi twalia, siwezi tena kusema,
Raisi punguza bei, iwe ndogo kama zama,
Shairi namalizia, waziwazi nikisema,
Wakenya tunaumia, mafuta yashuke bei.

Stephen Muia,
Malenga mneni(juja)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!