Nyuma ya Pazia

Kuna mambo yatendeka, huko nyuma ya paziya,
Jinsi yanavyofanyika, ni mbaya kuhadithiya,
Ila wapo wan’ocheka, eti wayafurahiya,
Yatawapata mabaya, hakika nawaambia.

Nyimbo zinazoimbika, ni mbaya kuzisikia,
Na vile zinachezeka, waama zinachefua,
Wanaimba na kuruka, huku wajikatikia,
Yatawapata mabaya, kuna siku yawajia.

Viongozi wa mashaka, huko nyuma wapo pia,
Yani wezi wa sadaka, hawamwogopi Jalia,
Wanasema kwa dhihaka, “nani atatuzuia”?
Yatawapata mabaya, wakigoma kusikia.

Japo mengi yafichika, sitaki kusimuliya,
Ukiona utachoka, hutataka kurudiya,
Miye hadi nachefuka, kila nikifikiriya,
Yatawapata mabaya, kama wasipotubia.

Wapo wanayoyataka, mbiyo wayakimbiliya,
Na makwao wametoka, waende yaangaliya,
Nyoyo hazinazo shaka, tuli kujituliziya,
Yatawapata mabaya, kama wasiposikia.

Ipo siku itafika, wengi wataijutiya,
Ambao sasa wacheka, siku hiyo wataliya,
Watakosa pakushika, wote hawatasaliya,
Yatawapata mabaya, heri wangenisikia.

Kalamu chini naweka, sitaki kuendelea,
Ninaacha kuandika, yachosha kuelezea,
Wan’ogoma kuokoka, jahimu waiendea,
Yatawapata mabaya, kama waking’ang’ania.

© Kinyafu Marcos, 2018.
MUUMINI WA KWELI

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!