Neswel Atakulinda

Tabasamu lako jema, kuliko chochote kile,
Wajulikana kwa wema, utendao huku kule,
Matendo yako ni mema, wasifiwa tangu kale,
Neswel* takulinda, takutunza sawa sawa.

Chochote ukitendacho, watenda kwa ufasaha,
Kiwe hiki ama hicho, matokeo ni furaha,
Waswahili chambilecho, katu huwa si karaha,
Neswel takulinda, takutunza sawa sawa.

Hata unapokosewa, huionyeshi hamaki,
Waficha ulotendewa, tadhani kawa haki,
Licha yako kuzomewa, mema huweki bureki,
Neswel takulinda, takutunza sawa sawa.

Maishani mwangu mwote, umekuwa kama nuru,
Iangazayo popote, penye giza pawe huru,
Pasi kuhofu chochote, upatikane uhuru,
Neswel takulinda, takutunza sawa sawa.

Furaha umezidisha, penzilo limekolea,
Mengi umeyawezesha, ushauri kunipea,
Mazuri hujakomesha, wazidi kunitendea,
Neswel takulinda, takutunza sawa sawa.

Sita nafunga shairi, ndipo pangu kituoni
Nitaileta mahari, hiyo ndiyo shukrani
Mola atupe umuri, tufurahi duniani
Neswel takulinda, takutunza sawa sawa.

© Ouma wa Opata

*Neswel ni ufupisho wa majina mawili; Agnes na Maxwel kuonyesha uhusiano wao

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!