Wanafunzi Someni

Likizo imeshaisha, shuleni mnarejea,
Nendeni bila mzozo, mpate kusoma poa,
Tutawapa nyinyi tunzo, mkipata gredi hai,
Someni nyinyi someni, mpate maisha mema.

Mngojao mtihani, siri ninawaambia,
Akili zenyu jazeni, na data ilo murua,
Vitabu vyote someni, bila data kusahau,
Someni nyinyi someni, mpate maisha mema.

Walimu wasikizeni, mtapata manufaa,
Maswali waulizeni, bila uoga haswaa,
Mtatoka ujingani, nanyi mtafurahia,
Someni nyinyi someni, mpate maisha mema.

Ondoeni wasiwasi, mtapata gredi poa,
Natabiri mtapasi, nasi tutashangilia,
Mtihani ni rahisi, pateni nyinyi kujua,
Someni nyinyi someni, mpate maisha mema.

Msiteketeze shule, isiwapate balaa,
Msiipige kelele, kuweni mmetulia,
Mtazipata kongole, nanyi tutajivunia,
Someni nyinyi someni, mpate maisha mema.

Ndimi malenga mneni, mengine siongezei,
Wekeni hayo moyoni, wanafunzi msomao,
Tutawaombea jueni, Mola Awasaidie,
Someni nyinyi someni, mpate maisha mema.

© Stephen Muia Musau
(Malenga mneni) Juja, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!