Dini Iliyo Safi

Yaeleza maandiko, asemayo Bwana Mungu,
Mawaidha ya mashiko, kwetu sisi walimwengu,
Katujuza na miiko, tusiwe changu ni changu,
Asema dini ya kweli, ni kufariji wagonjwa.

Ni kufariji wagonjwa, na walio vifungoni,
Nao wapate kuchanjwa, gonjwa litoke mwilini,
Wala wasije kupunjwa, wakatengwa majumbani,
Dini hii ndio safi, hufariji na yatima.

Hufariji na yatima, katika taabu yao,
Kuwaonea huruma, kila iitwapo leo,
Tusiache wakazama, wakavunja ndoto zao,
Dini hii ndio safi, inayojali wajane.

Inayojali wajane, na walozimia nyoyo,
Nao nuru waione, wayapate watakayo,
Kidogo na tugawane, zisitutawale choyo,
Dini hii ndio safi, safi iliyo safika.

Safi iliyosafika, ndio Mola aitaka,
Ile ilo thibitika, wala isiyo na taka,
Dini hii kwa hakika, haitutii mashaka,
Dini hii ndio safi, anayotaka Jalia.

Anayotaka Jalia, yeye Mkawini mbingu,
Dhahiri katuambia, katika vyake vifungu,
Vifungu vya biblia, kasema “shika wanangu”
Dini hii ndio safi, sote tuishike hiyo.

© Kinyafu Marcos
(Muumini wa Kweli)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!