Barua kwa Hayati Kinyata

Pokea salamu nyingi, hayati babu Kinyata,
Mepita miaka mingi, arubaini yapita,
Ni Mimi Githinji Mwangi, mambo mengi nayaleta,
Na Keki tuligawana, ila ilizua fujo.

Ni kweli sikukupata, Wala we hukuniacha,
Akilini nilijuta,haya wazi sikuficha,
Na Keki waliikata,ubinafsi kachacha,
Rais moi akawa, kipandeche aligawa.

Na moi aling’olewa, kwa makucha na majino,
Sijui ka alonewa, na wengi sio watano,
Hivyo ndo alisemewa,ati akala vinono,
Ndipo walipendezewa,rais yule kibaki.

Rais huyu kibaki,alipenda uwiano,
Na daima alibaki,kuchukia mizozano,
Akapigania haki, miaka ya kwanza tano,
Ila wakaja zozana, naye waziri mkuu.

Waziri mkuu Rao,alipenda kujiita,
Ni ukweli nisemao, kulizuka na matata,
Kwa ujinga tupendao, navyo vikaanza vita,
Ukabila kazalika, wacha watu wachinjane!

Baada ya dhiki raha, rafiki Kofi akaja,
Huyu ni Kofi Anani, akazileta faraja,
Kapatikana amani, pia katiba ya haja,
Kibaki akaondoka, mwanao tukachagua.

Huyu mwanao Uhuru, mwana kalandana nawe,
Akashika msururu, ili Keki aigawe,
Mimi ninamshukuru, na heshima apatiwe,
Aliupenda umoja, kachukia vya bwerere.

Nchi ina barabara, na treni za kisasa,
Wabinafsi twakera, tukidai zetu pesa,
Wanaficha zao sura,kwa yawapata mikasa,
Ndoto yako yatimia, nchi ya kujitawala.

Nimefikia kikomo, ni mimi wako swahibu,
Ni barua si mizomo, usipate kamwe tabu,
Umefikia mfumo, wa kukusemea babu,
Mimi mjukuu wako, za kweli zikufikie.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!