Ndoa ni Jambo la Baraka

Siku tuliyoingoja, na leo imewadia,
Nasi sote kwa pamoja, sherehe twafurahia,
Kauli yetu ni moja, baraka twawatakia,
Ndoa ni jambo la heri, mwende muishi salama.

Kila siku mpendane, ndoa iwe na furaha,
Tena mkashikamane, katika shida na raha,
Msisemane semane, ndoa ikawa karaha,
Ndoa ni jambo la heri, mwende muishi salama.

Kidogo ndicho cha kwenu, kikubwa msitamani,
Kisamvu twanga kwa kinu, kitenge kwako figani,
Hiyo ndo riziki yenu, ‘sitamani vya jirani,
Ndoa ni jambo la heri, mwende muishi salama.

Moyo wa mtu msitu, hao ndio walimwengu,
Msisikize ya watu, wengi wanayo majungu,
Wala msije thubutu, kuzivunja hizi pingu,
Ndoa ni jambo la heri, mwende muishi salama.

Upendo na utawale, nyumba ijae amani,
Achaneni na ya kale, hayana hata thamani,
Samahani iwe mbele, epukeni visirani,
Ndoa ni jambo la heri, mwende muishi salama.

Itunzeni yenu ndoa, wanetu twaambia,
Ndoa mkitia doa, siku mtajajutia,
Utajutia kuoa, ndoa ikawa udhia,
Ndoa ni jambo la heri,mwende muishi salama.

Twawaombea kwa Mola, akawalinde dawamu,
Awapatie chakula, na ndoa yenu idumu,
Wala msiache sala, hilo ni jambo muhimu,
Ndoa ni jambo la heri, mwende muishi salama.

© Kinyafu Marcos

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!