Dua Yangu

Nakuja kwako Manani, nipokee mja wako,
Nasali pasi utani, nasogea mbele zako,
Naomba nikiamini, nahitaji nguvu yako.

Hapa chini duniani, yapo mengi machafuko,
Insi wana visirani, na vingi vyao vituko,
Bila ya kwako Dayani, sitapata pambazuko.

Wewe tangu utotoni, ulinipa pendo lako,
Hata kwangu masomoni, ulifanya wema wako,
Bado ningali njiani, naomba rehema zako.

Kipaji changu cha nini, kama sina nguvu zako,
Na ningekipata lini, kama si kudura zako,
Najishusha hadi chini, ninanyenyekea kwako.

Uniongoze njiani, nipaone niendako,
Nitaingia shimoni, bila ya mwongozo wako,
Nisichekwe mtaani, nijaze neema yako.

Kaditama ukingoni, natuma maombi kwako,
Wewe wangu Mkawini, nasubiri jibu lako,
Kahari nakuamini, ma’na upo peke yako.

© Kinyafu Marcos,2018.
(Muumini wa Kweli)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!