Mama wa Kambo

Mama wa kambo ni mama, hata nae ni mzazi,
Apewe yake heshima, kama mwingine mlezi,
‘Sikae kumsakama, useme sie mzazi,
Mama wa kambo ni mama.

Kazi anapokutuma, kafanye bila ajizi,
Katu usije kugoma, fanya umalize kazi,
Na hiyo ndiyo hekima, aisemayo Mwenyezi,
Mama wa kambo ni mama.

Sikae kusemasema, ukawa nawe bazazi,
Kisa unazo ndarama, sasa ndo uwe mjuzi,
Laana utazichuma, ndugu nakwambia wazi,
Mama wa kambo ni mama.

Wengine wamsakama, na kumuona hawezi,
Wanamtwika lawama, hadharani waziwazi,
Hii si tabia njema, punguzeni upuuzi,
Mama wa kambo ni mama.

Ulezi hii karama, na wala haina kozi,
Hugawa yeye Karima, kuwapa wao wazazi,
Usije eti kusema, hufunzwa nao wajuzi,
Mama wa kambo ni mama.

Kama wayataka mema, mwana yatii malezi,
Muheshimu wako mama, bila ya kipingamizi,
Usimtende unyama, ukamtia banguzi,
Mama wa kambo ni mama.

Sisemi kwa kulalama, ila nakupa ujuzi,
Nakujuza wimawima, lisikupate tatizi,
Siku usije kukwama, kisa mama kizuizi,
Mama wa kambo ni mama.

© Kinyafu Marcos

Maoni 3

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!