Kapige Uzembe Vita

Huwezi fikia mia, kama hujaanza moja,
Utakwenda kwa hatua, kuikimu yako haja,
Kiwa wa kuriaria, kutimiza ni miuja,
Ukata kudadavua, kapige uzembe vita!

Kitamani kung’wafua, fanya afanyapo simba,
Kuwinda sijakwambia, jitahidi hata shamba,
Kazi ikikupotea, zifanye zozote ngwamba,
Ukata kudadavua, kapige uzembe vita!

Punda kasoro mkia, kaifanye yako kazi,
Kudusi humchukia, mja alo tegemezi,
Jasho kukudondokea, ndilo ataka mwenyezi,
Ukata kudadavua, kapige uzembe vita!

Kazi usijechagua, ukipata buti kaza,
Bora siwe maasia, Maulana kumkwaza,
Kuna unapofikia, bidii nayo kukaza,
Ukata kudadavua, kapige uzembe vita

© Justine Bin Orenge

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!