Walevi Mwanishangaza

Mwenzenu ninalo swali, lanitatiza hakika,
Laniuumiza akili, mawazo yananifuka,
Zama hizi maadili, ni wapi tumeyaweka?
Walevi mwapata nini, mnapotumia pombe?

Mwajazana gulosari, mpate vyenu vileo,
Mnazianza safari, mwonapo sasa machweo,
Hamuogopi hatari, jueni lipo tokeo,
Walevi mwapata nini, mnapotumia pombe?

Wengine kwenye vilabu, mnashinda hukohuko,
Hamna hata aibu, vilabuni mshindako,
Si shababi wala babu, wote ‘mekuwa vituko,
Walevi mwapata nini, mnapotumia pombe?

Afya zenu mwaharibu, ila wala hamjali,
Mwajibebesha adhabu, ‘tadhani ulevi mali,
Ulevi kwakweli tabu, hasa zile pombe kali,
Walevi mwapata nini, mnapotumia pombe?

Familia zateseka, pombe ndo kisababishi,
Kimamama wamechoka, kutazama matapishi,
Baba hebu badilika, sikia bila ubishi,
Walevi mwapata nini, mnapotumia pombe?

Nawe kijana wa sasa, leo sasa nakuhasa,
Embu ziache anasa, achana nazo kabisa,
Usizimalize pesa, kwenye pombe kujitosa,
Walevi mwapatani nini, mnapotumia pombe?

Ninawapa tahadhari, ziacheni hizo pombe,
Serengeti na safari, naye ndovu mwenye pembe,
Nawaomba tafadhari, msiponzwe na wapambe,
Walevi mwapata nini, mnapotumia pombe?

© Kinyafu Marcos

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!