Jitikise Kitaarabu

Nakuasi, ndugu penda burudani,
Fanya Kasi, kuchezea ulingoni,
Uwe mbisi, rukaruka maringoni,
Piga pasi,furaha masikioni,
Kuwa mbosi,rohoni na akilini,
Jitikise, uzame taarabuni.

Kaza nyaya, za gitaa kerezesha,
Ngoma piya, kwa makini kupigisha,
Furahiya, sauti kutetemesha,
We tembeya, we mutribu anzisha,
Cheza goya, usipende nakupasha
Jitikise,nyonga kuitikisisha.

Zoazoa, kiuno uje nengua,
Kuchomoa, staili ya kuua,
We zuzua, mtindo wa kudengua,
Kanyagia, ukibandikabandua,
Inamia, huku kupangapangua,
Jitikise, ukinyakuanyakua.

Kwenye baa, gongo ukilimimina,
Tupa baa, wimbo kutibu tibana,
Tenga saa, nasa wakuburudana,
Gaagaa, ki hila songeleana,
Kupagaa, wabaki kuulizana,
Jitikise, wimbo chezeka chezana.

Ukitaka, utazame runingani,
Pasi shaka, usomee kitabuni,
Chapikika, hata kwenye gazetini,
Tabulika, ndani ndani rungoyani,
Tikisika, barani na baharini,
Jitikise, tulia taarabuni.

Taarabu,yaondoa mzuzuo,
Kwa mhibu, yamshikisha sikio,
Taratibu, kupunguza upumuo,
Na karibu, ikwondolee kilio,
I sababu, wimbo kuupa chaguo,
Jitikise, asteste si mbio.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!