Shilingi

Ehe shilingi ya ng’ara, yang’arika kama mwezi,
Mwenye shilingi ni bora, hela ya mpa mzizi.

Shilingi ya mpa mja, kijoyo kichaguacho,
Mwenye hela mwenye haja, huwapa akitakacho.

Shilingi ya maajabu, huuza roho ya mja,
Pamoja kwongeza tabu, ‘hijui dhiki faraja.

Hela ina upumbavu, kupofua mja mwema,
Shilingi ina uvivu, usone kazi i njema.

Hela ina maskio, huchagua kusikiza,
Hela itakuja mbio, kwa yule alopendeza.

Shilingi ina miguu, kukimbia kwa bwanyenye,
Tena yapiga maguu, maskini imfinye.

Hela kweli ni msasi, kusaka imtakaye,
Humtoroka kwa Kasi, mja imchukiaye,

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!