Mwisho wa Mbivu

Moyoni sina Uchungu,
Bali ninazo huzuni,
kwa kuwa muhibu wangu,
Amenifanya ni duni,
Limekua pendo langu,
Kwake halina Thamani.

Nyonda ni wangu Mwalimu,
Alonifunza kupenda,
Mpaka nikafahamu,
La usawa na la inda,
Na kwako sijakhitimu,
Huwaje pendo kuvunda.

Japo Akufukuzae,
Huwa hakwambii toka,
Bali Taona mamboye,
Ghafula mebadilika,
Nyonda Tamweka iye,
Moyo bado wamtaka.

Kwake nyumbani kifika,
Anganiona si kitu,
Ni kwamba naukumbuka,
Wema wake Wa kiutu
Nashindwa kumbanduka
Pendo Angatia Kutu

Baiti Tano takoma,
Mengi yafilie ndani,
Kwake sitorudi nyuma,
Japo Niko matesoni,
Tazidi omba karima,
Nami niwe Furahani.

© Omar Rajab
(Mombasa, Kenya)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!