Nuhu Bakari U Wapi?

Napiga mbiu ya mgambo, nikiwaita wahenga,
Hili nijibiwe jambo, hata kama kwa uganga,
Lisiwe Motoni tumbo, jibuni nyie malenga,
Wajua Nuhu Bakari, ‘alenda’ sayari gani?

Hili jijambo ni gogo, ni zito kwenye mtima,
Ewe Kimani Wa Mbogo, unijibu himahima,
Nipe wakaa kidogo, unijibu kwa heshima,
Wajua Nuhu Bakari, ‘alenda’ sayari gani?

Huyu pasua kamanda, simpati kwenye soko,
Shinikizo la nipanda, nifae mwinyi mbokoko,
Kwa vile nilimpenda, alipotungia huko,
Wajua Nuhu Bakari, ‘alenda’ sayari?

‘mefika wa kulalama, nipate huyu mtunzi,
Sitaki ‘baki lawama, nihangaike ja panzi,
Ombi Vikita Mulama, nelezee kwa mapenzi,
Wajua Nuhu Bakari, ‘alenda’ sayari gani?

Okwetiso viniceti, nakutuma kwa tadhima,
Hizi nimepanga beti, ujumbe ninautuma,
Unijibie kwa hati, nitajiweza kusoma,
Wajua Nuhu Bakari, ‘alenda’ sayari gani?

Enzi zile kipindini, kamusi ya changamka,
Kitulia sebuleni, Jumamosi kidamka,
Na Khaemba Wafulani, kumtafuta nataka,
Wajua Nuhu Bakari, ‘alenda’ sayari gani?

Kwenye milima ya safu, hata mabondeni kwingi,
Kapanga safari ndefu, ni Mimi Githinji Mwangi,
Ewe Yakobo Kinyafu, ‘metuma wangu utungi,
Wajua Nuhu Bakari, ‘alenda’ sayari gani?

Jicho nimelisinzia, mwenzangu napiga mwayo,
Ninaomba kuwambia, ya Nuhu machache hayo,
Bakari ukimjia, ‘apo’ salimia huyo,
Wajua Nuhu Bakari, ‘alenda’ sayari gani?

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!