Tiba Yakinifu

Tiba ilo yakinifu, inayoondoa ujinga,
Inayotoa uchafu, na akili kuiganga,
Hoja zikae kwa safu, kichwani zikijipanga,
Maarifa vitabuni, huzitibu zetu bongo.

Huzitibu zetu bongo, watu wakwite kipanga,
Ukayapange malengo, vipi uweze jijenga,
Ikunuoe kama nyengo, usiwe ja butu panga,
Chakula chake ubongo, chatolewa kitabuni.

Chatolewa kitabuni, chakupa afya hakika,
Chakutoa taabani, adha isije kushika,
Soma uchimbue ndani, ndipo utafaidika,
Kazi bila maarifa, ni meli bila nahodha.

Ni meli bila nahodha, chombo huenda mrama,
Hupatwa na nyingi adha, mwishowe huweza zama,
Na shida kadha wa kadha, huwa zinakisakama,
Epuka adhabu hii, anza leo kujituma.

Anza leo kujituma, ujijenge sawasawa,
Jilazimishe kusoma, paukwa pawe pakawa,
Mbeleni usije kwama, ukabakia mkiwa
Kamata kitabu sasa, ujinga uweze koma.

© Kinyafu Marcos

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!