Buriani Bett

Habari za tanzia, tumezipata hakika,
Ni habari za kilio, gwiji wetu katoweka,
Ajali imemuua, Wakenya twasikitika,
Pumzika palo wema, ewe Nicholasi Betti.

Dhahabu ‘katuletea, alikuwa msifika,
Kwa kasi alikimbia, akawa atambulika,
Japo ametangulia, tumwombee kwa Rabuka,
Pumzika palo wema, ewe Nicholasi Betti.

Ameacha familia, pamoja na wake kaka,
Alikuwa na bidii, vyema alifahamika,
Kwa kuwa katangulia, tuishi kumkumbuka,
Pumzika palo wema, ewe Nicholasi Betti.

Bendera nusu zikae, twomboleze mtajika,
Dua njema tumwombee, mbiguni apate fika,
Naye apate tulia, huko kwema kwa Rabuka,
Pumzika palo wema, ewe Nicholasi Betti.

Kalamu yangu yalia, chini nami naiweka,
Nicholasi twakwombea, wewe pata pumzika,
Nanyi wanafamilia, nguvu awape Rabuka,
Pumzika palo wema, ewe Nicholasi Betti.

© Stephen muia Musau,
(Malenga Mneni) Juja, Kenya

Maoni 3

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!