Nachukia

Nachukia, wafisadi wa nchini,
Nachukia, utabaka humu nchini,
Nachukia, ugomvi huko nyumbani,
Na haswaa, ajali barabarani.

Nachukia, ukoloni mambo leo,
Nachukia, shule zinapoungua,
Nachukia, ugonjwa unapoua,
Na haswaa, waja kuwa na tamaa.

Nachukia, watu kutowajibika,
Nachukia, hekima kupuuzika,
Nachukia, nyumba zinapoanguka,
Na haswaa, haki kukandamizika.

Nachukia, wanyongwe kunyongwa sana,
Nachukia, wanandoa kuachana,
Nachukia, wapenzi wano pigana,
Na haswaa, wale wanao uana.

Nachukia, mashamba kunyakuliwa,
Nachukia, misitu kuharibiwa,
Nachukia, makaa yanapochomwa ,
Na haswaa, miti mipya kutopandwa.

Nachukia, maji safi nikosapo,
Nachukia, usalama ukoswapo,
Nachukia, wizi uongezekapo,
Na haswaa, wezi watuibiapo.

Nachukia, wanodharau maskini,
Nachukia, wajivunao kazini,
Nachukia, wenye viburi vichwani,
Na haswaa, walo na wivu nyoyoni.

Nachukia, watu waso na hisia,
Nachukia, wasiofwata sheria,
Nachukia, wale waso fikiria,
Na haswaa, wanaopenda ghasia.

Nachukia, wapendao sana pesa,
Nachukia, waso kubali makosa,
Nachukia, wanaopenda kukosa,
Na haswaa, waibao zetu pesa.

Nachukia, walio na mapuuza,
Nachukia, mengine mimi kwongeza,
Nachukia, shairi kulipunguza,
Na haswaa,shairi kulimaliza,

© Stephen Muia
(Malenga Mneni) Juja, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!