Mungu Akulaze Nicholasi

Nimepata mshituko, kupotea kwa jagina,
Siwafanyii vituko,nasema wazi mchana,
Tumempoteza huko, shujaa huyo kijana,
Mungu akulaze pema, pema Nicholasi Beti.

Ajali haina kinga, ajali ‘hina’ kafara,
Maozi tumeyafunga, wana pwani wana bara,
Wanandi na wana Tanga, tunalilia hasara,
Mungu akulaze pema, pema Nicholasi Beti.

Kenya ikawa tajika,kwa mbio zako za Kasi,
Kenya ikatajirika, riadhazo Nicholasi,
Rekodi ikavunjika, Afirika na Urusi,
Mungu akulaze pema, pema Nicholasi Beti.

Ni Beinjing’i uchina, mwaka wa kumi na tano,
Hakika uling’ang’ana, ukazidi mkazano,
Mbioni ukashindana, huu ukweli si ngano,
Mungu akulaze pema, pema Nicholasi Beti.

Tukikulaki uwanjani, kwa sima na murusiki,
Kwa nyimbo zikisheheni, kujitoma kwa mziki,
Ukabamba shereheni, bila wasi wala dhiki,
Mungu akulaze pema, pema Nicholasi Beti.

Ya Jibana ndio mengi, ya watu tu ni uneni,
Twazipiga dua nyingi, uwe na Mungu peponi,
Sumu ni maneno mengi, nimefika kikomoni,
Mungu akulaze pema, pema Nicholasi Beti.

© Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!