Tutapatana Debeni

Kiongozi mwadilifu,ni vigumu kupatika,
Kwa sababu ni wachafu,kila mara wageuka,
Wao ja fisi wachafu,wenye pupa iso katika,
Kwenye karamu ya fisi,yupi mlafi zaidi.

Viongozi hawa kweli, huhalalisha haramu,
Na yale yalo halali, wanasema ndo haramu,
Ndo wafaidi kwa mali,naswi wanatuhujumu,
Kwenye karamu ya fisi,yupi mlafi zaidi.

Wengine hupoka mali, bila kujali wenyewe,
Viwanja vya shule kweli, hudai ndio wenyewe,
Na vyeti viso halali, wanatoa tuonyeshwe,
Kwenye karamu ya fisi, yupi mlafi zaidi.

Wataivunja katiba,bili iwafae wao,
Wagurume kama simba, watutishe tukimbie,
Kisha wajenge majumba, na makasri huko kwao,
Kwenye karamu ya fisi, yupi mlafi zaidi.

Hawajengi barabara, wajali matumbo yao,
Mikono yao Imara, kupoka kiso chao,
Na watwitishapo kura, watajenga hutwambia,
Kwenye karamu ya fisi, yupi mlafi zaidi.

Maji hatuna nyumbani, nao ‘kahidi kuleta,
Kwa sasa haonekani, simuni hatumpata,
Tunaishi hali duni, mwokozi hatujampata,
kwenye karamu ya fisi, yupi mlafi zaidi.

Uongozi umewalevya, kasahau miaka tano,
Kwa kutuongoza vibaya, kura atapata tano,
Nasi tutashangilia, kwa kumkata mikono,
kwenye karamu ya fisi, yupi mlafi zaidi.

Hivyo mafisi skieni, shairi namalizia,
Karamu yenyu acheni, mpate tutumikia,
‘kifika tena debeni, sisi tutawachagua,
Kwenye karamu ya fisi , yupi mlafi zaidi.

© Stephen Muia
(Malenga Mneni) Juja, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!