Balaa Itawapata

Nilizipata habari, tokea kule shuleni ,
Shule zimo kwa hatari, zawashwa moto gizani ,
Nini hasa mwafikiri, muwashe moto shuleni ,
Balaa mwaitafuta, na kweli itawapata.

Sikieni wanafunzi,mlipelekwa shuleni ,
Mkapewa moja kazi, msome vitabu tani ,
Nayo ni rahisi kazi, isiwashinde jamani ,
Shule mnapozichoma, balaa itawapata ,

Shule mkizichoma, mwatuvuruga vichwani,
kwani mwafaa kusoma, mkiwa huko shuleni ,
Lakini sio kuchoma, msomeako jamani ,
Balaa mwaitafuta, na kweli itawapata.

Msiwe na wasiwasi, mtapita mitihani ,
Msiwe kama waasi, maovu kuyatamani ,
Mitihani ni rahisi, wanafunzi kumbukeni ,
Shule mnapozichoma, balaa itawapata .

Sisi wazazi twalia, machozi yamo machoni ,
Tabu mmetuletea, mkiwa bado shuleni ,
Nanyinyi mtalipia, kwa kuyachoma mabweni ,
Balaa mlitafuta, na kweli itawapata .

Simama wima simama, utweleze hadharani ,
Bada ya skuli kuchoma, umepata raha gani ,
Umepata yepi mema, ya furaha maishani ,
Shule mnapozichoma, balaa itawapata.

Mengine sitaongeza, kalamu naweka chini ,
Nikiwaomba kuwaza, hasa walio shuleni ,
Shule kuteketeza, faida yake ni gani? ,
Balaa mlitafuta, na kweli itawapata.

© Stephen Muia Musau
(Malenga Mneni) Juja, Kenya

Maoni 2

  1. revochatus n limwecha

    mi napenda kukupa shukurani za zati kwa kuandaa kazi zuli kama hizi zinazo nifundisha mimi na jamii zetu kwa ujumla sina budi kusema sana mungu akulinde na akupe afya zuli mpaka milele ameen

    Jibu

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!