Ndege Wangu

Mie nimepata ndege, ni mrembo ndege huyu,
Huyu si ndege bwege, amshinda mbayuwayu,
Miguu hana matege, Wala ya mang’ombo huyu,
Anazo rangi sufufu, na usimwite tausi.

Na usimwite tausi, urembo wake wazidi,
Anazo mbio za Kasi, avunja mbuni rekodi,
Ajua vyema densi, haswa pasipo hasidi,
Tabia ajua kwiga, ila yeye si kasuku.

Ila yeye si kasuku, apenda kwishi na mie,
Huchekesha sote sisi, kwa vituko azidie,
Simwite chiriku asi, kelele asipigie,
Ndege huyu ni mpole, usimseme ni njiwa.

Usimseme ni njiwa, na haishi vichakani,
Na hawezi kunasiwa, na kwa la kwako tunduni,
Ni mkali kichezewa, kushinda mwewe angani,
Hupaa kwenye mawingu,ndege huyu si kipungu.

Ndege huyu si kipungu, Wala hana papatio,
Kiumbe toka kwa Mungu, ndege huyu ni mkeo,
Hizo ni hisia zangu, kuwatunza tupendao,
Mwanamke ndege mwema, liko ndege wa dunia.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!