Mja Acha Unafiki

Ewe mja mzandiki, unaefanya dhihaka,
Watoa ukidhihaki, na sifa tele wataka,
Wadhani watapa haki, misifa un’ojiweka,
Mja acha unafiki, Mola hapendezwi hivyo.

Wasaidia wajane, huku ukijionyesha,
Kila mtu akuone, kile ulichofikisha,
Sitaki nikutukane, ila unanichefusha,
Mja acha unafiki, Mola hapendezwi hivyo.

Vikongwe nao yatima, wawapa kwa mashariti,
Inawauma mitima, kisa hizo zako noti,
Neno la Mungu lasema, toa pasina shuruti,
Mja acha unafiki, Mola hapendezwi hivyo.

Kwenye nyumba za ibada, huko wala sipagusi,
Waitoa misaada, kwa kejeli na matusi,
Mja watafuta shida, wajivutia mikosi,
Mja acha unafiki, Mola hapendezwi hivyo.

Mja nakuhasa mja, mja acha unafiki,
Hii ndiyo yangu hoja, mja hauambiliki,
Mja kweli ipo haja, rudi katafute haki,
Mja acha unafiki, Mola hapendezwi hivyo.

Epuka hizo ndarama, zisikupe majivuni,
Ukajifanya ni mwema, hapa chini duniani,
Siku utaja kuzama, kwa moto wa jahimuni,
Mja acha unafiki, Mola hapendezwi hivyo.

© Kinyafu Marcos

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!