Usikate Tamaa

Tuliianza safari, tuende tunapokwenda,
Adha zilitukabiri, tukachoka kama punda,
Ila leo mahodari, vikwazo tumevishinda,
Safari yetu yasonga, mwendo tunauongeza.

Safari yetu yasonga, mwendo tunauongeza,
Kila siku twajiganga, mawazo mema kuwaza,
Hii kwetu ndio kinga, katu tusije teleza,
Mbele tutazidi kwenda,kurudi nyuma ni mwiko

Mbele tutazidi kwenda,kurudi nyuma ni mwiko,
Milima tutaipanda,hadi tufike twendako,
Malengo tutayalinda, tusijeitwa vituko,
Nia nayo yetu haja,hatima wote tufike.

Nia nayo yetu haja,hatima wote tufike,
Pamoja twajikongoja, ukingo tukaushike,
Safari yetu ni moja, tujikaze tusichoke,
Mbele huko ni patamu,kuliko tulipotoka.

Mbele huko ni patamu,kuliko tulipotoka,
Sote bora tufahamu, haipo haja kuchoka,
Lisogee gurudumu,mwisho liweze kufika,
Kwa uweza wa Dayani,mkono atatushika.

Kwa uweza wa Dayani,mkono atatushika,
Nia tuweke moyoni,pasipo kutetereka,
Hatutakwama njiani,hadi kitaeleweka,
Sasa na tujipe moyo,juhudi tuzidi weka.

Sasa na tujipe moyo, juhudi tuzidi weka,
Tufanye tuyatakayo, bila chini kubweteka,
Tusiikubali choyo, siku ije kututeka,
Twendeni jamani twende, safari tutaifika.

© Kinyafu Marcos

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!