Moto wa Kifuu

Mwendani merudi tena, nalo jambo la kusema,
Mefikiri tena sana, juma baada ya juma,
Najaribu kukazana, nchini si tena kwema,
Unawaka mwingi moto, Kama Moto wa kifuu.

Kwenye vyombo vya habari, hakukomi haya mambo,
Wengi ni wa Moja bari, ndoa zinakwenda kombo,
Shatoboa hii Siri, mesema wazi si fumbo,
Unawaka mwingi moto, Kama Moto wa kifuu.

Hasira ndio hasara, wahenguzi waligonga.
Hasara ni kwa hasira, mababuze waligonga,
Sitaki kamwe kukera, Wala useme naringa,
Unawaka mwingi moto, kama moto wa kifuu.

Mume awasha mioto, kuchomea familia,
Haogopi hilo joto, Wala wana kulilia,
Awapiga vichwa ngoto, kisha wanajifilia,
Unawaka mwingi moto, kama moto wa kifuu.

Wake siwaachi nyuma, si tungo la kuongoa,
Mwakata waume nyama, viungo kuwanyofoa,
Nyote mwaliana njama, Maisha kuyapogoa,
Unawaka mwingi moto, kama moto wa kifuu.

Hakuna mja kamili, sote tuna zetu ila,
Fikiria mara mbili, usiishi kwa ufala,
Tumia zako akili, kazini na ukilala,
Unawaka mwingi moto, kama moto wa kifuu.

Nondokea zangu beti, za nasaha zote saba,
Jitulize kwenye kiti, na yote yako nasaba,
Usitumie kijiti, waarifu kwa mahaba,
Unawaka mwingi moto, kama moto Wa kifuu.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!