Nataka Nisome

Babangu ninaumia, medhoofika na siha,
Masomoni najutia, siyo kwamba ni mzaha,
Nimeshindwa kutulia, siioni mie raha,
Baba nataka nisome, fadhili elimu yangu.

Visa ninavyopitia, nimechoka kuviona,
Wenzangu wanichekea, naonwa mjalaana,
Karo hujanilipia, kwani mie si wa mana?,
Baba nataka nisome, fadhili elimu yangu.

Baghalani angalia, tunaishi maskini,
Niwazapo ninalia, tutengwapo kijijini,
Kuchao ni kibarua, nalo jembe mabegani,
Baba nataka nisome, fadhili elimu yangu.

Wana umetukopoa, nikiwa mmoja wao,
Cha nne nimepitia, nimefuzu nenda chuo,
Wa tisa wakaribia, nitazame kweli Leo,
Baba nataka nisome, fadhili elimu yangu.

Abu kweli fikiria, kaditama nimefika,
Nimeshinda nikilia, na kuchekwa nimechoka,
Jaribu kuendelea, pale nina amefika,
Baba nataka nisome, fadhili elimu yangu.

© Hosea M Namachanja
Milembe-Bungoma

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!