Umependa Pesa Zangu

Leo nimekugundua, hunipendi msichana,
Ulipo wanichezea, hunioni wa maana,
Chochote nachokwambia, hukioni cha dhamana,
Mrembo hujanipenda, umependa pesa zangu,

Nikosapo hasa pesa, mawi unanitendea,
Wanizulia mikasa, nisoweza kukimbia,
Sijui yangu makosa, kupenda binti bandia,
Mrembo hujanipenda, umependa pesa zangu,

Unonapo na ndarama, unajifanya mzuri,
Unakuwa wa heshima, japo weye ni hatari,
Usione mie mwema, unichezee kamari,
Mrembo hujanipenda, umependa pesa zangu,

Nimechoka nimechoka, meumia vya kutosha,
Kwa sasa ninakuruka, mrembo umenichosha,
Mkata nina mashaka, sitaki kunipotosha,
Mrembo hujanipenda, umependa pesa zangu,

Kaditama nikienda, elewa nimekujua,
Mahaba yamenishinda, pindi nakuangalia,
Ninaogopa kukonda, kwa yale nayapitia.
Mrembo hujanipenda, umependa pesa zangu.

© Hosea M Namachanja
Milembe, Bungoma, Kenya

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!