Maskini Mie

Ole maskini mie, niso nguvu za kuteta,
Naomba mnijalie, mwache kunipiga vita,
Kipita mnangalie, mkome kunipa tata,
Maskini Mimi chungu, ni uchungu chungu nzima.

Ukumbuke wema wangu, wema wa faida kwenu,
Maandiko na mafungu, kwenye maabadi yenu,
Muige tabia zangu, mtie bidii zenu,
Maskini Mimi chungu, ni uchungu chungu nzima.

Kiwa kwenye harakati, kusaka yangu makuli,
Ninapata atiati, kwona kikubwa kivuli,
Ninasimama tisti, kukanyagwa kwa makali,
Maskini Mimi chungu, ni uchungu chungu nzima.

Nikikwea kiambaza, na kuchupia jikoni,
Ulimi naulambiza, kwenye vyombo sukarini,
Kwa chuvi mwanifukuza, ama moto kuchomeni,
Maskini Mimi chungu, ni uchungu chungu nzima.

Kipata njema sehemu, ya kujenga fungulima,
Na kumbe ni mumu humu, mingi miwa umelima,
Wanipulizia sumu, na kunichimba kwa uma,
Maskini Mimi chungu, ni uchungu chungu nzima.

Mkata Mimi mdudu, kwa nini ya kuonewa,
Mie dhaifu kidudu, sina kamwe kupendewa,
‘Nomba’ ninaye abudu, awafanye kunelewa,
Maskini Mimi chungu, ni uchungu chungu nzima.

© Mwangi wa Githinji.
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!