Usafi Mwilini

Nasugua kwanza meno, nisije nikawaudhi,
Nitatumia mikono, na hiki kijiburashi,
Nisugue yangu meno, nisije nikawaudhi,
Usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni.

Tuzingatieni waja, usafi kwetu mwilini,
Ni jambo lilo la hoja, kulifanya maishani,
Kwani latupa umoja, twongeapo umatini,
Usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni.

Usafi jambo muhimu, tupate ‘lizingatia,
Usafi pia kwa damu, ndilo jambo la murua,
Hatoroki binadamu, ukiwa safi sikia,
Usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni.

Mwilio wapumzika, usafi ‘kizingatia,
Uchovu unapunguka, nawe unafurahia,
Makwapa kutokunuka, ni jambo la kusifia,
Usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni .

Nenda kapate kukoga, upate jasho fukuza,
Kabla kung’oa nanga, ukenda kujitembeza,
Ili usiwe na woga, hata liingiapo giza
usafi jambo muhimu , waja tuzingatieni .

Magonjwa yanotusibu, haswa kama huku nchini,
Uchafu ndio sababu, twadhurika miilini ,
Kwa hivyo piga hesabu, jiondoe uchafuni,
Usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni .

Usafi tuzingatie, hata kwetu majumbani,
Maji safi tutumie, hata kule hoteleni ,
Nazo taka tuzizoe, tukazitupe jaani,
usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni .

Wadudu kwetu nyumbani, tutapata kuondoa,
Mende panya kabatini, tutaweza kuwaua,
Hivyo usafi wendani, tupate kuuvamia,
Usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni.

Usafi utatufaa, tukizingatia waja,
Ina tele manufaa, tudumishe kwa pamoja,
Hivyo basi tunafaa, wote uchafu kuvunja,
Usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni .

Kalamu nabwaga chini, ya moyoni nimesema,
Ndimi malenga mneni, alezaliwa kusema,
Kusema yalo ya ndani, ambayo yana hekima,
Usafi jambo muhimu, waja tuzingatieni.

© Stephen Muia Musau
(Malenga Mneni) Juja

Maoni 2

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!