Mbona Mwanitesa?

Ninawaomba ruhusa, enyi wazazi wa Phibi,
Mbona mnanitesa, mwaninyima mimi Phibi,
Mimi sikufanya kosa, kumpenda binti Phibi,
Nioneeni huruma, nampenda Phibi sana.

Nampenda Phibi sana, Wazazi nisikizeni,
Nasisi tunapendana, tumewekana nyoyoni,
Siwaelewi bayana, na mmfungie ndani,
Hamtaki tuonane, wala anione yeye.

Wala anione yeye, nyi hamtaki kabisa,
Sezi kuumiza yeye, hata akifanya kosa,
Sana anipenda yeye, akinikosa ni kosa,
kubalini tupatane, hasa akiwa nyumbani.

Wasa akiwa nyumbani, niiteni nitakuja,
Niseme yalo moyoni, twongee moja kwa moja,
Mjue sina utani, ‘tamposa siku moja,
Phibi nampenda sana , niwe naye kubalini.

Niwe naye kubalini, apate pia furaha ,
Najua yupo shuleni, yuasoma kutwakucha,
Naomba ‘kiwa nyumbani, mmwache nimpe raha,
Nitoleeni upweke, Yeye ndiye nitaoa.

Yeye ndiye nitaoa, awe wangu wa halali,
Hivyo msinichukie, tutapata sisi mali,
Rununu mrudishie, niwe namjulia hali,
Mengine sitaongeza, Shairi namalizia .

Shairi namalizia, nikimuomba Jalali,
Anipe mke murua, mwenye mapendo ya kweli,
Nanyi wazazi mjue, mapenzi ni ya wawili ,
Hasa wanaopendana, kama Phibi na Stivini,

© Stephen Muia Musau
(Malenga Mneni) kutoka Juja

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!