Nyama Tamu Nyama Chungu

Mwenzangu nakutajia, usichirizie mate,
Kuna nyama nakwambia, humwagisha mja mate,
Yabidi kuilambia, vidole vyako vyote,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Ukikaanga chunguni, uchemshie jikoni,
Ubanikie motoni, tokose sufuriani,
Uikaushe juani, uhifadhi firijini,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Viongozi wa taifa, maamuma wa imamu,
Babu wenye maarifa, mapadire maasumu,
Wachezaji na marefa, wandalizi wa karamu,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Walonavyo,wasonavyo, ni nyama ilo halali,
Fikiri vile ilivyo, ukitia pilipili,
Nakwomba sipike ovyo, usiitie ukali,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Ukitaka kuchongewa, tu kwa nyama hiyo yako,
Usitake kuonewa, nyamayo iso ukoko,
Usiombe kuchekewa, usipate na sijiko,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Kipata mwanasiasa, na mifuko ya siasa,
Anavyo vingine visa, itabidi kuwaasa,
Mumuchague kisasa, na wengine mtatesa,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Kihudhuria maziko, ukiwa wote shajaa,
Na vilio navyo viko, nyama ya kupa tamaa,
Hamwishi kweli vituko, hawataki kunyamaa,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Tukila nyama na Keki, ya harusi kwa furaha,
Nyama haileti dhiki, ni raha pasi karaha,
Jifanyie tahakiki, lisani nyama ya raha,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Ulimi huna mfupa, mwenzangu unielewe,
Ni mawaidha nakupa, jihadhari usilewe,
Ulimi wajaza pupa, hupaa kuliko mwewe,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Mwenzangu ninanyeshewa, mejikunjia jamvi,
Sitaki niende pewa, Wala nizue gomvi,
Maneno yote elewa, Ku mema na vivi hivi,
Lisani ni nyama tamu, lisani nyama i chungu.

Mwangi wa Githinji
(Malenga wa mchanga Kati)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!