Wanafunzi Wakigoma

Wataimba kwa kejeli, popote waandamane,
Waibadilishe hali, wendapo wafuatane,
Hawajali watafeli, wakipandacho wavune,
Wanafunzi wakigoma, athari huwa ni nyingi.

Shule zao watachoma, hasara kadha wa kadha,
Hawatauona wema, wanapoharibu fedha,
Hawaijali lawama, wala yoyote mawaidha,
Wanafunzi wakigoma, athari huwa ni nyingi

Wataudhi kwa tabia, wasijali la heshima,
Bora iwe yao nia, bila kutenda hekima,
Tena wazifunge njia, ama magari kuchoma,
Wanafunzi wakigoma, athari huwa ni nyingi.

La msingi ni mzazi, atende wake wajibu,
Aitende yake kazi, ya kuwafunza adabu,
Jambo kuu ni malezi, kwa mzazi ajaribu,
Wanafunzi wakigoma, athari huwa ni nyingi.

Wazazi lenu tendeni, msiwachie mwalimu,
Wafunze humo nyumbani, ili heshima idumu,
Waongoze kanisani, maadili wafahamu,
Wanafunzi wakigoma, athari huwa ni nyingi.

Tuungane watu wote, kulea na kukosoa,
Taadhima ifuate, migomo kuiondoa,
Jamii njema tupate, pasipo na kubomoa,
Wanafunzi wakigoma, athari huwa ni nyingi.

Wanafunzi msomeni, muwache mengi makeke,
Mtafakari shuleni, ya bidii muyaweke,
La muhimu ni amani, hakika ieleweke,
Wanafunzi wakigoma, athari huwa ni nyingi.

Tuvikomeshe vishindo, tuangazie elimu,
Twataka mema matendo, waja wanaoheshimu,
Mzaha tuweke kando, ya elimu tufahamu,
Wanafunzi wakigoma, athari huwa ni nyingi.

© Kĩmani wa Mbogo
(Mwanagenzi Mtafiti)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!