Dawa za Kulevya

Nakataa katakata, kujipaka hino taka,
Na mdomo sitofyata, kwa risasi ngenifyeka,
Wallahi hutonipata, zino dawa kuzishika,
Katu dawa za kulevya, situmie asilani.

Huanza kama mzaha, toti moja toti mbili,
Mwisho ikawa usaha, kuacha kitendawili,
Furaha kawa karaha, kakosa afia mwili,
Katu dawa za kulevya, situmie asilani.

Msukumo wa marika, mara nyingi huchangia,
Wengi wakadanganyika, katekwa bila kujua,
kadhani ndo kuchanuka, kumbe kaburi wangia,
Katu dawa za kulevya, situmie asilani.

Kijinga hudanganyika, kwa mairungi na bangi,
Eti utaerevuka, moshi kimeza kwa wingi,
Nakuchanua chanuka, haina faida bangi,
Katu dawa za kulevya, situmie asilani.

Vijana ndo hatarini, kutumia na kuuza,
Si kokeni si heroni, kisirini kusambaza,
Kama juisi chupani, sokoni pia shuleni,
Katu dawa za kulevya, situmie asilani.

Dawa hizi huharibu, ndugu yangu akiliyo,
Ukasahau vitabu, kadorora matokeyo,
Usafi kawa taabu, ukakosa zingatiyo,
Katu dawa za kulevya, situmie asilani.

Wazazi mna jukumu, wanenu kuwelekeza,
kuwafundisha nidhamu, na njia njema sikiza,
Ya ukweli wafahamu, mapema bila kusaza,
Katu dawa za kulevya, situmie asilani.

© Bonface K. Wafula
(Mwana wa Tina) Nakuru

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!