Mafuriko

Mola wangu Mola wangu, sikia changu kilio
Kwa kweli nina machungu, hasaa ninaumia
Ikubali dua yangu, niache mimi kulia
Twende wapi Mola wangu , Mafuriko yatuua?

Baraka mvua Mungu, ulipata kutupea
Shamba tukapata Mungu, mavuno tukangojea
Lakini mvua Mungu, hasara ‘metuletea
Twende wapi Mola wangu, Mafuriko yatuua?

Wa huko Tana wenzangu, yawahamisha mvua
Kila siku ni machungu, maji yawapa kilio
Mvua mekuwa sugu, watu kadha imeua
Twende wapi Mola wangu, Mafuriko yatuua?

Magari yao wenzangu, yamesimama kwa njia
Yamekwama Mola wangu, sababu ya hi mvua
Nakuomba Mola wangu, izamishe hii mvua
Twende wapi Mola wangu, Mafuriko yatuua?

Yamewasomba wenzangu, haya maji ya mvua
Yamewaua wenzangu, zinalia familia
Mola wangu Mola wangu, tutolee hii baa
Twende wapi Mola wangu, Mafuriko yatuua?

Bwawa la Solai Mungu, lilivunjika sikia
Likaua wenzangu, hauwaoni mamia
Nakuomba Mola wangu , kilio changu sikia
Twende wapi Mola wangu , Mafuriko yatuua?

Moyoni nina machungu, mengine sitanenea
Nakuomba Mwenyezi Mungu, twondolee hii baa
Nifurai na wenzangu, daima Tukusifie
Twende wapi Mola wangu, Mafuriko yatuua?

© Stephen Muia Musau

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!