Nataka Kwenda Shuleni

Nataka kalamu, niende shuleni,
Kitabu muhimu, na sare nipeni,
Mwambie mwalimu, sikai nyumbani,
Nipe nina hamu, ya kwenda shuleni.

Mimi niamke, ndoto sitamani,
Nyumbani nitoke, vitu mfukoni,
Mfuko nishike, nitoke nyumbani,
Njia nishike, niende shuleni.

Nikute mwalimu, mle darasani,
Nitoe kalamu yangu mfukoni,
Anipe mwalimu, mwongozo wazoni,
Mengi ya muhimu, nipate shuleni.

Ujinga utoke, ule wa nyumbani,
Vema niandike, changu kitabu,
Elimu nishike, mle darasani,
Darasa nitoke, na cheti shuleni.

Aidha hakimu, niwe maishani,
Nipate hatamu, nendamu mbungeni,
Mwema mwanadamu, niwe maishani,
Nikiwa mwalimu, nifunze shuleni.

© Kimani wa Mbogo

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!