Tukulanga Mwanangu

Sikiliza kwa makini, kisa changu nakironga
Kisa hiki cha huzuni, cha kijana Tukulanga,
Mwana huyu wa mjini, alifunzwa zote kunga,
Tuku kijana mdogo, aliyeharibu sifa.

Kijana wa Kinyamwezi, alezaliwa mjini,
Aliyepewa malezi, makubwa yenye thamani,
Akaona hayawezi, akazama mtaani,
Huko yaliyompata, sisahau asilani.

Tuku akiwa mdogo, babaye nilimkanya
Nilimpa na kipigo, ila bado alisonya,
Akayapa na kisogo, yote niliyomuonya,
Akayaona si kitu, babaye ninayofanya.

Alianzia jikoni, kufunua sufuria,
Akahamia chumbani,kudokoa mia mia,
Akaficha mkobani, skuli ‘ende tumia,
Tabia akaipenda, sasa ikawa ya kwake.

Siku zilienda mbele,na kundi akaliunda,
Kawa tena si mpole, Tuku kageuka nunda
Kaiba hadi mchele, kijana akatushinda,
Tuku sasa hashikiki,nyanya kapata simanzi.

Tabia ikapevuka, katafuta na bunduki,
Kuta zote kaziruka,mwana tena hashikiki,
Mtaani kasemeka,kijana sio riziki,
Watu wakakaa kimya,shuhuda washudie.

Arobaini kufika, la kuvunda likavunda,
Duka kaenda kuteka, kwa bwana Juma Mponda,
Wakora nao ‘kafika, piga risasi ya panda
Ubongo ukamwagika,mauti ikamfika.

Kwetu kukawa msiba, turubai tukafunga,
Tuku alikosa tiba, hadi kwa wote waganga,
Mauti ilimbeba, hata bila ya kupanga,
Sikio aliliziba, mabaya yakamkuta.

Watu wakakusanyika, msiba kushuhudia,
Pamoja twende kuzika, Tuku kaaga dunia,
Huzuni ilitushika, Tuku tulimuhusia,
Tuku kafukiwa chini, udongo umemmeza.

Huo moto wa jahimu, ndio aliutafuta,
Ile ya shule ilimu,hukutaka kuifwata,
Babaye hukuneshimu, ufidhuli akaleta,
Sasa leo hatunaye,huzuni imetupata.

Mamaye amlilia, uchungu u mtimani
Jonzi alilomwachia, aje ampoze nani
Na wadogo zake pia, wanalia si utani
Buriani Tukulanga, sasa amebaki jina.

Hatunalo la kusema, huzuni imetufika,
Nyoyoni limetuchoma, wala hatuwezi cheka,
Mola tujaze hikima, yako tuweze yashika,
Tusiishi kama Tuku, jahimu ikatufika.

© Kinyafu Marcos (Muumini wa Kweli)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!