Sioti Tena Mchana

Nakana sitorudia, kuota nimetosheka,
Tangoja kujilalia, katika wangu mkeka,
Ujapo umechakaa, talala nikipinduka,
Sioti tena mchana, ndoto kumbe ni hadaa.

Naota ni Marekani, kiamka ni Dandora,
Tena nala jalalani, kama kuku kichakura,
Melalia sakafuni, baridi sawia chura,
Sioti tena mchana, ndoto kumbe ni hadaa.

Naota mevaa koti, kwenye ndege ninashuka,
Mfukoni ni manoti, madola ya Amerika,
Nasomwa kwa magazeti, redioni kitajika,
Sioti tena mchana, ndoto kumbe ni hadaa.

Naota mejishindia, milioni kwenye Loto,
Watu wanishangilia, kwa vifijo moto moto,
Ghafla najipindua, mkekani viroboto,
Sioti tena mchana, ndoto kumbe ni hadaa.j

© Boniface Wafula
(Mwana wa Tina) Lanet, Nakuru.

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!