Utamu wa Ngonjera

Ngonjera ni ushairi, ulio na pande mbili,
Hoja huwekwa dhahiri, wajenga watu wawili,
Kila pande hufikiri, ikichekecha akili,
Tungo hii ya ngojera, ni tungo ya kuvutia.

Yahitaji ubunifu, uweze kutunga beti,
Ili zikae kawa safu, mtunzi ajizatiti,
Sio iwe tungo chafu, yenye nyingi shotikati,
Tungo hii ya ngojera, itunge ukitulia.

Huanza kwa malumbano, baina ya mbili pande,
Wote huchangia neno, hadi mmoja ashinde,
Mwisho waunga mikono, azimio wakatende,
Tungo hii ya ngonjera, inahamsha hisia.

Malumbano yakizidi, utamu ndo huibuka,
Kila mtu na juhudi, kilele aweze fika,
Hadhira wana faidi, hoja zinavyopangika,
Tungo hii ya ngojera, huchoki iangalia.

Namimi najitahidi, beti jaribu andika,
Mwenyewe hapa shahidi, kilele sijakifika,
Katu siwi mkaidi, juhudi zahitajika,
Tungo hii ya ngonjera, wajuzi wajitungia.

© Marko John Kinyafu

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!