Rehema Zake Rabuka

Riziki mpaji Mungu, hugawa kwa wanadamu,
Hutoa fungu kwa fungu, kwa waja tulio humu,
Twafurahi walimwengu,bhakika riziki tamu,
Kudura zake Rabana, hazina mipaka kamwe.

Yeye ndiye anagawa, kwa huyu hata kwa yule,
Kila mtu anapewa, huyu hiki yule kile,
Mola mtoa vipawa, kwake vimejaa tele,
Kudura zake Manani, wala hazichunguziki.

Tuyapatapo magumu, katika haya maisha,
Yeye hushika hatamu, na njia kutuonyesha,
Hakika kila sehemu, Mwenyezi anatuvusha,
Kudura za Maulana, azijuaye ni yeye.

Anaweza kutuvusha, hata tusipo taraji,
Katika yetu maisha, Mola yeye ndo mpaji,
Waama anatutosha, Mungu wetu mu’mbaji,
Kudura zake Raufu, kwakweli zatushangaza.

Nanyi msiomwamini, hebu leo geukeni,
Kwani mnangoja nini, Manani kumuamini?
Mtangoja hata lini, au mmepewa nini?
Kudura zake Karima, hakika zitawatosha.

Wala msiwe na hofu, na mashaka mioyoni,
Yeye Mungu mtukufu, bado anawapendeni,
Atawafuta uchafu, mkae mwake rahani,
Kudura zake Dayani, zote zitawasafisha.

Sisi tumeshuhudia, makubwa na ya ajabu,
Kwa alivyo tujalia, sasa twastaajabu,
Dunia kuiambia, kweli tunayo sababu,
Kudura zake Jalia, kwa kweli tumeziona.

Tutazidi kuzisema, kila siku maishani,
Tungali hivi mapema, tukiwapo ujanani,
Tutasifu wake wema, tuuseme hadharani,
Kudura zake Jalali, zipo peke yake zizo.

© Marko John Kinyafu

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!