Nabii Hakubaliki Kwao

Watu walimtabiri, toka zamani za kale,
Wengi walimsubiri, wayathibitishe yale,
Alikuja nayo heri,
Heri ilo na uzuri, wa uzima wa milele
Yeye ndo mfano bora, nasi tujifunze kwake.

Alikuwa Mungu kweli,aleshuka duniani,
Uungu wake asili, makao yake mbinguni,
Alihubiri injili,
Injili ile ya kweli, ili tutoke dhambini,
Yeye ndo mfano bora, nasi tujifunze kwake.

Alitenda miujiza, miujiza mingi sana,
Kila aliloliweza, kafanya bila hiana,
Kwa nguvu zake muweza,
Muweza alimjaza, naye akawa Rabana,
Yeye ndo mfano bora, nasi tujifunze kwake.

Wengi walijiuliza, sasa vipi huyu bwana,
Yale aliyoeleza, mbona ni magumu sana,
Wakabaki wanawaza,
Wakawaza na kubeza, nakuona hana ma’na,
Yeye ndo mfano bora, nasi tujifunze kwake.

Kweli aliieleza, kwao ikawa bayana,
Maswali walimwuliza, ili wajue kwa kina,
Wengine walipuuza,
Walipu’za na kuzoza, na kumkashifu sana,
Yeye ndo mfano bora, nasi tujifunze kwake.

© Kinyafu Marcos
(Dar-es-salaam,Tanzania)

Tafadhali usikose kuongeza Maoni yako kuhusu shairi hili.

Baruapepe yako haitaoneshwa hadharani. Maeneo yenye alama * ni lazima yajazwe!